SIMULIZI YA MSAMAHA WA MAMA – 08 - Chumba Cha Mapenzi -->

SIMULIZI YA MSAMAHA WA MAMA – 08


Lilikuwa swali zito sana kwake kulijibu, machozi yalimtiririka kama baadhi ya wanafunzi ambao walikuta matokeo ya siamini wakashindwa kujizuia na kuangua kilio.
Hakuweza kuamini alichokiona Seid, maswali mengi yaliingia kichwani mwake, akawa na msongo wa mawazo, alihisi presha kupanda na kushuka ghafla, taratibu alianza kuanguka chini na kupoteza fahamu, wenzake waliokuwa karibu walimdaka wakampeleka chini pole pole akiwemo kijana mmoja aliekuwa swahiba wake wa karibu aitwae Hamad…
Songa nayo……
“Subirini kwanza muacheni apate hewa, au tafuteni kitu mumpepee!. Nini kimetokea?.
Yalikuwa maneno ya Ticha ambae ndie aliempatia majibu ya mapema seid. baada ya kuingia eneo hilo. Aliuliza kimetokea nini?. Wanafunzi walimjibu kwa kumuambia kafika hapa akiwa anasema nimeshinda nimeshinda, anaangalia matokeo tunaona mtu anaanguka chini.
Ticha hakujibu kitu chochote, alisogea mpaka kwenye ubao yalipokuwa yamebandikwa matokeo, namba ya seid alikuwa anaijua vizuri sana, alivaa miwani akaanza kusoma namba moja baada ya nyingine mpaka alipoipata namba ya Seid. Nae pia hakuamini alichokiona, jasho lembamba lilianza kumtoka, alitikisa kichwa akaachia msonyo wa kushangaa, wanafunzi wakauliza vipi ticha?.
Ticha aliwaangalia wote waliokuwa wamesimama mbele yake.
“kwa hiki nlichokiona ana haki ya kuzimia, na kwa namna hii hakika Tanzania haitoendelea maisha yote. Alisema.
“Unatufumba mwalimu wangu una maana gani?. Aliuliza Hamad ambae alikuwa ni rafiki wa karibu mno na Seid, alikuwa na furaha zake za kufaulu, alikuwa moja ya vijana wa watu wakubwa ndani ya nchi ya Zanzibar.
“Nna asilimia mia matokeo ya seid yameuzwa. Ticha maneno yalimtoka kwa hasira.
“Unamaanisha nini mwalimu.
aliuliza tena kijana huyo hamad. Aliekuwa mfupi mwenye asili ya kiarabu na upara wa dizani aliokuwa akipenda kuupaka mafuta.
“Inauma sana lakini haina haja ya kujua kwa sababu hata mkijua hamtosaidia chochote, Mungu atasaidia tu nshallah. Ticha aliongea kwa uchungu.
“Mwalimu ukifanya hivyo Wallah utakuwa umetuacha njia panda, tena utakuwa unatukosea sana, we ndo ulikuwa ukitupitisha mambo ya misemo kila siku na kutupa habari za ushujaa wa william mwandishi mkongwe kutoka Uingereza. Nakumbuka uliwahi kutuambia maneno haya ambayo nayakumbuka sana yanauozungumzia ushujaa wake.
** Wanadam wako wa aina nne tofauti katika hii dunia, ukiwajua hakika utaishi vizuri, aina ya kwanza watu ambao wanafurahi kuona maendeleo ya wenzao yanarudi nyuma hasa wanyonge, na dawa ya mtu ambaye unahisi anaitaji kurudisha maendeleo ya mtu nyuma, ni kuongea mabaya yake aliyoyatenda.
Mwalimu ulizungumza maneno haya ila baadhi ya wanafunzi watakuwa wameyasahau kwa sababu ulitumia kifaransa, mimi niliyashika ili badae yaje yanisaidie, nilivyoiangalia hii picha naona kabisa Seid atakuwa amekosewa, ukiwa kama msemaji mkuu wa wiliam inakuwaje unashindwa kuzungumza ukweli!?. Ticha wewe ni mwalim mkubwa hapa chuo, wanafunzi wengi wanakufahamu na wana kukubali kutokana na kazi yako nzuri ya ufundishaji, vipi unaonekana kuwa mnyonge baada ya kuwatetea wanyonge?.
Hamad aliongea maneno yaliyoonekana kumgusa Ticha, ticha moyo wake ulifunguka na kuitaji kuwaambia ukweli, kabla ya kuanza Seid aliamka akiwa kama mtu aliechanganyikiwa, walijaribu kumtuliza lakini hakutulia, alimuangalia Ticha na kumuuliza.
“Nakumbuka ulinipigia cm mbele ya mama yangu na kuniambia nimefaulu, inakuwaje hata matokeo ya chet sipati? ulikuwa unantania?
Alivyozungumza tu kila mtu alijua kabisa mshkaji kadata, ticha alikaa kimya akashindwa la kuongea, kijana Hamad ambaye alimkumbusha maneno ya wiliam mwandishi wa misemo maarufu nchini uingereza, alimuangalia Ticha wake akavua miwani na kumuomba ajibu swali la Seid.
Seid alimtolea ticha macho, tayari akili zake hazikuwa sawa, Ticha aliwangalia wanafunzi kijasho chembamba kikiwa kinamvuja.
” Seid ni mwanafunzi mwenzenu na ni mwanafunzi ambaye wengi wakisikia kafeli watashangaa sana, Ila hayo ndo matokeo yaliyopo kwenye ubao na ndio maana nimesema kwa namna hii Tanzania hatutoendelea kwa sababu, kabla ya hapo niliyaona matokeo ya Seid na alikuwa amepata matokeo ya juu sana, kwa hiyo sielewi imekuwaje. Alisema.
” Una maanisha matokeo ya Seid yameuzwa?. Hamad alimuuliza Ticha.
“Yeah.
“Waaoo!. Seid my friend, Hamad alimgeukia seid akamshika begani huku akimuita, wewe ni mnyonge. Yeah wewe ni mnyonge rafiki yangu.
kuna walimu wako ngazi za juu wanaujua unyonge wako hapa shule, na wameamua kucheza huu mchezo ila usijali, nakuahidi kabla ya mipango ya kuingia chuo haijaanza, matokeo yako yatarudi. Naomba nikuahidi hilo. Alisema kwa kujiamini.
“Hamad. Wewe ni rafiki yangu sawa. Na umenisaidia vingi sana sikatai, unadhani utanisaidiaje juu ya hili.?.
Seid aliuliza huku machozi yakimlenga lenga.
” Babaangu ni mtu mkubwa sana serikalini, na anapenda sana kutetea haki za wanyonge, nimesoma na wewe miaka mitatu, naijua hali yako ilivyo mbaya na unategemea kitabu kikusaidie katika maisha. Haina haja ya kuchanganyikiwa, wewe ni rafiki yangu nitakusaidia na matokeo yako utayapata tu, I Promise you.. alisema hamad.
Seid alishusha pumzi kidogo akili zake zikakaa sawa. Hamad alikuwa akimpenda sana mshikaji, ukoo wake wote ulikuwa ukoo wa wasomi, kuanzia mababu zake mpaka ndugu zake wote wana elimu zao za kutosha. Hali ngumu ya maisha aliyokuwa nayo Seid aliifahamu vizuri kwa sababu seid hakujificha shuleni maisha yake halisi, alimweleza kila mmoja kuwa yeye ni masikini na anategemea kitabu kuja kumtoa. Hali ilipelekea kupata baadhi ya misaada japo wapo waliomcheka, lakini hamad alimueshim sana na kumchukulia kama moja ya ndugu zake wakubwa na anaowaeshim.
Alipomaliza kumpa moyo seid alimgeukia mwalimu na kumuomba wasogee yeye na seid pembeni waongee private ( secret conversation). mwalimu alikubaliana kila kitu na hamad kwa sababu nae alikuwa na mawasiliano ya karibu sana na Seid. Walienda wakakaa chini ya mti wa pambo la shule na kuongea zaid ya nusu saa, mwisho hamad aliwaomba wote wawili waingie kwenye gari lake waende kiwengwa shamba alikokuwa akiishi seid kwa ajili ya kumpeleka, kwani alijua kabisa rafiki yake hayuko sawa wakimuachia aende peke yake na usafiri wa dala dala anaweza asifike.
Hamadi alikuwa anapenda kuongea English na kifaransa kuliko lugha yoyote ile ulimwenguni, upo muda kiswahili kilikuwa kinampiga chenga kwa alivyozoea kingereza na kifaransa, alikuwa na upendo kwa kila mmoja lakini kwa Seid ulipitiliza, alimkubali sana seid kwa sababu alikuwa ni kijana mwenzake anaependa kitabu, pia amezungukwa na shida ambazo huwa hazifichi kwa kila mtu, huku akibukua darasani ili siku moja aweze kuokoka kimasikini kutokana na kitabu.
Alihakikisha anakuwa nae makini kwa karibu sana ili apate vitu zaid kutoka kwake kuhusu Kitabu, Pia Hamad ni mtu aliependa sana kufatilia maisha ya mashujaa wa hapa duniani, watunga mashairi pamoja na misemo, ziliiva sana na seid pamoja na mwalimu waliezoea kumuita Ticha kwa sababu na wao pia kuwa watu wanao penda sana mambo hayo.
Kutokana na bara bara za Zanzibar hasa ziendazo shamba kukosa magari ya kusababisha foleni, walitumia dakika 30 pekee kufika kiwengwa, walipaki gari mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi seid, Bi najma aliposikia sauti ya gari ilibidi atoke ndani, kufika mlangoni akaona sura ngeni zimeongozana na mtoto wake, hakushtuka kwa sababu aliona ni vijana wenzake pia wanaonekana wanatoka mjini.
Seid aliwakaribisha sana sehemu anayoishi na mama yake, walikaribia kwa kuingia ndani huku wakimsalimia bi najma.
“Jamani karibuni sana.
Bi najma aliongea akivuta kisturi na kukaa mbele ya Ticha na Hamad waliokuwa wamekaa kwenye mkeka.
“Tushakaribia mamaangu, tushakaribia sana wala usijali. Alisema Hamad.
“E bhana karibuni ndugu zangu hapa ndo nyumbani, hamad kila nlipokuwa nakwambia twende nyumbani hukuitaji ila leo umefika. Alisema Seid.
“Heheheeee usijali rafiki yangu uenda Mungu bado alikuwa ajapanga.
“Au na wewe ulitaka kuwa kama Deniss Rwadsh alivyofanya kwa mbwa wake?. Aliuliza seid.
“Hahahahaaaaa Seid umeanza mambo yako, wewe mtu una matatizo sana Akyamungu mimi unifananishe na Deniss?, yule alikuwa kiumbe chengine myahudi yule. Alisema wakacheka. Ila kabla hatujaendelea ebu kwanza tuongee na mama, mama! vipi hali,alimgeukia Bi najma akamuangalia na kumuuliza hali yake.
“Salama babaangu, hawajambo huko?. Aliuliza bi najma.
“Mama!. Seid alimuita mama yake kabla hamad hajajibu.
“Abee mwanangu
“Huyu anaitwa hamad mwanafunzi mwenzangu, na huyu ni Mwalimu wetu tunapenda kumuita professa, kichwa kizima kimejaa Elimu hiki kione hivyo hivyo kilivyo..
Mwalimu aliachia tabasam baada ya kuitwa professa, akashika kichwani huku akisema “Hamna bhana wako maprofessa sio mimi.
” karibuni sana. aliongea bi najma akiwakaribisha kwa mara ya pili.
“asante mama tushakaribia. Alisema hamad.
” Nimefurahi sana kuwafahamu, ila naomba mnisamehe maana hapa ndo hakunaga hata kinywaji chochote zaid ya maji tu.
” Mama usijali sisi tuko sawa, tuko sawa kabisaaa yani usijali kabisa mamaangu.
“Nadhani nilikuaga naenda mjini asubuhi kuangalia matokeo. Seid aliiingilia kati.
“ndio mwanangu vipi?
” Ah mamaangu acha tu nilichokikuta huko ndio kimefanya marafiki zangu hawa wafike hapa.
Alimuambia kila kitu kilichotokea mjini, mwalimu na hamad nao walichangia kumuelewesha mama ili asiwe na presha juu ya mwanae, walimuahidi lazima sheria ichukue mkondo wake na lazima matokeo ya seid yarudi hayawezi kwenda kirahisi rahisi tu kama inavyokuwa inatokea kwa wengine.
Walizidi kuongea mengine mengi ambayo yaliwafanya wacheke sana na kufurahi, walipoona muda unaenda ilibidi waage kwa ajili ya kuondoka, Hamad alitoa wallet yake akatoa elfu 30 na kumpatia Bi najma.
“Mama angu hizi hapa zitasaidia japo sabuni.
“Eh! asante babaangu, asante sana! mungu akubariki uwe na roho iyo iyo baba!. Alisema kwa furaha bi najma.
“Usijali mama haya ndo maisha yakitanzania japo wengi wanasahau hili, ila mshairi mmoja wa kifaransa anasema hivi:. kwa nini msahau asili yenu wakati mkiiendeleza mtaishi kwa furaha kuliko mkiiga ya wageni?, mimi ni mfaransa, hata nitajirike vipi bado nitaikumbuka ufaransa, najua kuna mataifa yameendelea na wanaiona ufaransa ni nchi masikini, ila siwezi kuisahau hata nitajirike vipi kwa sababu na mimi nimezaliwa kwenye umasikini. unajua alimanisha nini hapo huyu jamaa mamaangu?. Alisema kisha kumuuliza swali bi najma.
“sijui! mambo ya wasomi hayo.
“Heheheee, wewe ni mamaangu kwa sababu unaweza kunizaa na umenizalia rafiki yangu kipenzi.
Huyu jamaa alivyomanisha mfano wake ni hivi, maisha ya kitanzania ni maisha ya kimaskini, Mtanzania ataekuambia mimi natokea kwenye ukoo wa matajiri huyo muongo, Akyamungu huyo muongo mama!, kama wewe ni tajiri basi jua kuna vibabu vyako huko nyuma vimeishi kwenye nyumba za makuti. Mamaangu mimi hapa naishi kwenye familia ya wasomi, Yeah naweza kusema hivyo kwa sababu familia yangu yote ni ya wasomi na baadhi ya ndugu zangu wana hela nyingi sana, Je! hali hii inipelekee mimi kusahau asili yangu ya kitanzania Kisa nimezaliwa kwenye Pesa nisahau kuwa asili yangu ni ya kimasikini?. Aliuliza.
“Hapana, Bi najma alijibu.
“Basi mi ngoja nikuage mama tuondoke kama jibu unalo.
Aliinuka akiwaacha wote wako kwenye kicheko cha machozi kutokana na maongezi yake, Bi najma nae alisimama akamshukuru sana kwa msaada wake na kumshukuru pia kwa kumuahidi kufatilia zoezi la mwanae, waliinuka wote wakatoka mpaka nje huku bi najma akisema karibuni sana jamanii, na wao waliitikia kwa kusema asante, wakaingia kwenye gari na kuanza safari ya kwenda mjini.
Seid na mama yake walisimama nje mpaka gari lilipoishiliza, Bi najma alinyoosha mikono juu kumshukuru Mungu.
“mama vipi? Aliuliza seid.
” Mwanangu elfu 30 kubwa sana kwangu mungu ambariki huyu kijana mashallah.
” Mama!, Hamad ni rafiki yangu mkubwa na amenisaidia sana kiukweli huko shule. Alisema Seid. Waliingia ndani wakiwa bado wanaendelea kuongea.
Wakati wao wanaingia ndani upande wa pili Hamad na Ticha wakiwa njiani wanarudi mjini ghafla walikutana na gari nyeusi imezuia bara bara mbele yao, walipata mshangao sana wakapunguza mwendo kisha wakasimama, upande alikokuwa amekaa Ticha alitokea mtu amevaa nguo ya kumfunika uso wake kama gaidi akamtandika Risasi Ticha na kutoeka. Alikimbia fasta mpaka kwenye gari hilo leusi lililokuwa limezuia bara bara kwa mbele akaingia ndani na kukanyaga mafuta, tairi zilizungushwa, rami ikasuguliwa vizuri jamaa akatoeka kimuundo huo akimuacha ticha katika wakati mgumu wa jeraha, risasi ikimpatia maumivu makali mno ya kushindwa kustahimilia na kupoteza fahamu.