Jifunze namna unavyoweza kupenda tena baada ya kuachwa
October 18, 2019
Edit
Katika suala la uhusiano wa kimapenzi, hakuna kanuni maalumu ambayo itakupa jibu la moja kwa moja kwamba, uhusiano uliokuwapo utadumu milele au la. Bali unapokuwa kwenye uhusiano huo njia pekee ya kukupa matumaini ama imani ni kwa njia ya kumuomba Mungu.
Kwa mantiki hiyo, ikitokea mpenzi uliyenaye akakuacha wakati ukiwa bado unampenda kwa dhati, swali la kujiuliza ni je, huyo uliyenaye ndiye mpenzi Mungu aliyekupatia? Kutokana na swali hilo itakufanya upate imani ya kutokata tamaa, kwa sababu ya ukweli kwamba, Mungu ndiye mwenye kujua aina ya mpenzi ambaye atakufaa katika maisha yako.
Kwa jinsi hiyo, kama ulishawahi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi ambao ulitamani udumu milele, ikatokea umevunjika kutokana na mambo kutokwenda sawa, pengine mwenzi wako alikuwa anakunyanyasa, anakudanganya kwa kutoka na michepuko. Au anakupiga, siri zako anazitoa nje na kukuongelea vibaya kwa watu wengine na mwishoe akaamua kukuacha, usikate tamaa bali endelea kumuomba Mungu.
Ni katika juhudi za namna hiyo, itakufanya uwe mtu mwenye furaha wakati wote, kwa sababu hakuna binadamu aliyezaliwa akaacha kutembea kutokana na kuanguka. Ama kuacha kulala usingizi kutokana na kuota ndoto mbaya. Elewa kwamba, maisha hayapo sawa siku zote. Hata katika suala la uhusiano wa kimapenzi ipo hivyo.
Huwezi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi wakati wote ukiwa mwenye furaha bila ya kujua maumivu yake yalivyo. Na huwezi kuyaelewa mapenzi ya dhati bila ya kujua hisia za mtu aliyeachwa zikoje. Ni vizuri ujifunze kupenda tena baada ya kuumizwa. Usiweke sana moyoni jambo hilo mpaka kufikia kuumia au kuumwa, kwa sababu maisha ya kimapenzi hayatabiriki, ni kama kifo. Unaweza kupanga jambo unalotaka liwe hivyo unavyotaka liwe, lakini likawa tofauti na matarajio yako.
Usikate tamaa. Tambua kwamba, uhusiano mbaya ndiyo unaosababisha mtu aumie moyo na wala si mapenzi. Kwa hiyo ni vyema ukajifunza kutokana na makosa. Pia unachotakiwa kujua siku zote ni kwamba, kuvunjika kwa uhusiano uliokuwepo ni kama kufunguliwa mlango kwa njia nyingine ya uhusiano. Jitahidi tu kutokuchukua muda mrefu kuufungua mlango huo, pamoja na kwamba, uamuzi ni wako kuruhusu mwingine kukupenda au kumpenda.
Jitahidi sana kutovunjika moyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, wapenzi wengi wakishaachwa husema hakuna mapenzi ya kweli. Suala hilo si kweli, na usijaribu kumwambia mtu mwingine neno hilo, kwa sababu tu umeumizwa wewe. Kwani wapo wapenzi wengi ambao wamepitia matatizo kama hayo zaidi ya mara moja akiachwa na wapenzi tofauti, lakini mwishoe anafarijika baada ya kupata mpenzi mpya mwenye mapenzi ya dhati.
Huyo akamsababisha asahau machungu yote ya awali. Akamfanya awe mtu mwenye furaha moyoni. Na kubwa zaidi akamuonyeshea kile alichokuwa akikitamani siku zote katika maisha yake. Kwa namna nyingine, mpenzi anatakiwa akubaliane na ukweli kwamba, uhusiano uliopita umebaki kuwa historia. Na kwamba, ipo tena nafasi nyingine ya kuruhusu furaha na tabasamu zuri kwa mtu mwingine akupende ama umpende.
Usikae ukawa mnyonge, ukajilaumu, ukatukana, ukalaani kutokana na jinsi mambo yalivyotokea. Usikae kujaribu kila wakati kujiumiza moyo na kumpigia simu kumtafuta mtu ambaye pengine alishasahau penzi lako, ukijipa moyo na kuendelea kumuomba msamaha ukifikiri atakusamehe. Tambua kwamba, mpenzi akishakusahau na kuanza uhusiano upya na mtu mwingine si rahisi kukumbuka kurudisha penzi lenu mkaendelea kupendana kama ilivyokuwa awali. Zaidi anaweza kukudanganya na kuendelea kukutumia kama spea ya gari.
Cha msingi, kama umeachwa jipange upya kwa kuangalia wapi ulikosea ili usirudie tena kosa hilo.
Asante sana na Mungu awabariki wanaotaka kubarikiwa