Mume wangu amejua kuwa namsingizia mtoto, lakini pia ameshindwa kumkataa - Chumba Cha Mapenzi -->

Mume wangu amejua kuwa namsingizia mtoto, lakini pia ameshindwa kumkataa

Nimeolewa miaka 14 iliyopita. Nilikutana na mwenza wangu mkoa flani baada ya mimi kupangiwa kituo cha kazi mkoa huo, kwa kipindi hicho mwenzangu yeye alikuwa anasimamia biashara za baba yake nami nilikuwa ni mwalimu.
Ilikuwa siku za weekend natengeneza ubuyu, karanga na visheti naweka kwa wenye maduka ya vyakula wananiuzia kwa makubaliano maalum ili kujiongezea kipato, mmoja wa wateja wa karanga alikuwa ni huyu mwenza wangu na hapo ndipo tulianza mahusiano na hatimaye tukafunga ndoa.
Baada ya ndoa alijitoa kusimama kazi za baba yake na baba yake akampa mtaji kama asante ya kile akichokifanya, kwa kuwa alikuwa tayari anajulikana kibiashara tulifungua biashara ya duka la nguo akawa anasimamia yeye na mimi nikaendelea na kazi yangu.
Biashara yangu ya karanga na ubuyu ilizidi kuimarika na nikawa nasambaza mpaka kwenye mini supermarkets zilizoko hapa mjini, mtaji wangu ukakuwa tukakubaliana tuongeze nguvu kwenye biashara ya mume wangu, nayo ikaimarika ikabidi tuajiri vijana ili kuongeza nguvukazi.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja ndoani sikubahatika kubeba hata mimba, nikawa najiambia tu kwamba kuzaa ni majaliwa, siku moja nikamgusia mwenzangu kuhusu mtoto, nisikie kama na yeye ana hamu ya kuwa na mtoto, akasema tufanye kazi kama mtoto yupo atakuja tu, miaka ikasogea tukiwa tunafanikiwa kwa hili na lile, ila hatukujaliwa kupata mtoto jambo ambalo lilikuwa linanisononesha lakini kwa mwenzangu sikuona kama anajali.
Baada ya miaka mitatu nikamgusia tena habari ya mtoto, nikamwambia tuende Hospitali kwa check up, labda kuna tatizo, akasema nenda kacheki wewe, matatizo ya uzazi mnakuwaga nayo nyie wanawake, nikaona isiwe tabu, nikamshirikisha wifi yangu mkubwa ambaye kiumri ni mtu aliyekuwa na 35 kipindi hicho, akanishauri kuwa sio mbaya nikapima mimi ili nijue, akanitania labda mumeo tayari ana watoto wanaomtosha, tukacheka. Baada ya siku mbili nikaomba ruhusa kazini nikienda Hospitali, ni mbali Mkoani kwa sababu sisi tuko wilayani. Nilimpigia simu dada yangu akanisindikiza kwa sababu nilishawahi kumshirikisha sononeko langu kuhusu haja ya kuwa na mtoto.
Tulifika Hospitali na tukapewa appointment ya kumuona Dr wa kina mama, nilifanyiwa vipimo nikaambiwa kuwa sina tatizo, Dr akaniuliza kama mme wangu alishawahi kuwa na mtoto nikamwambia kuwa sina taarifa ya yeye kuwa na mtoto, akashauri labda na mume wangu naye akapate vipimo, nikamwambia kuwa nitamfahamisha na yeye apime, kichwani nikakumbuka majibu yake ya awali. Baada ya pale niliwasiliana na mwenzangu kumjulisha majibu ya kipimo pamoja na ushauri wa Dokta, akasema Dokta hatoi mtoto njoo nyumbani. Nilirudi nyumbani nikiwa na sononeko, nikajiambia kuzaa ni majaliwa, maisha yakaendelea.
Nilijaribu kuwa namkumbushia baada ya vipindi flani, mwishowe akaanza kuwa mkali, mama yangu na ndugu zangu wakawa wananitafutia dawa za miti shamba ninywe, wengine wanasema labda kuna mirija imeziba, wengine wanasema labda nina chango la uzazi, nikanywa dawa nikachoka nikaacha.
Nilizidi kushangaa kwa sababu sio ndugu zake na wala sio yeye alijali kuhusu mtoto, hata wifi na shangazi zake ambao nilijaribu kuongea nao wamshauri tukapime tupate tiba waliniambia tu niombe Mungu. Tumepiga hatua kubwa ya mafanikio ya kiuchumi, nimepeleleza labda mwenzangu ana mtoto lakini hakuna niliposkia jambo kama hilo.
Mwaka juzi mama yangu, dada na shangazi zangu waliniita nyumbani kwa ajili ya hilo jambo, tukakaa pamoja tukashauriana na kukubaliana kuwa nitafuta mwanaume anayeshabihiana na mume wangu kwa kimo, au sura na rangi nijaribu kutafuta mtoto kwake, kuna kaka mmoja japo mdogo kwangu nikaona kuwa ana wajihi unaolingana na mme wangu, huyu kijana ni Dokta (Medical assistant), kwa ile hamu ya kuwa na mtoto ambaye angalau atakuwa mrithi japo wa kimagumashi sikuona shida kumtokea huyu kijana.
Nilianza mazoea naye kidogo kidogo, japo salamu na tabasamu pana, akanizoea, siku moja tukatoka outing na kijana nje ya mji, nikamuweka wazi akanielewa, basi seminar za uongo na kweli zikawa hazikauki, na kwa sababu ya biashara mume wangu anasafiri sana, so nikawa na nafasi ya ku enjoy na damu changa.
Mungu si athumani useme ataniwekea kinyongo kwa sababu nime cheat, mwezi wa pili kwenye mahusiano na dokta nikanasa mimba.
Nilijikuta natokwa na roho ya ubinadamu juu ya mume wangu, nilijikuta hata akisafiri naomba Mungu hata agongwe na gari asirudi tena. Nikajikuta kila baya natamani limpate. Aliijua hali yake, akabaki kunizuga. Baada ya kupata mimba ile, tulishauriana na kijana dokta ahame pale wilayani, ili kikinuka nisimtie kwenye matatizo, na nilijiambia lolote liwalo nitapambana na huyu zoba(my husband)
Kijana aliwasiliana na uncle yake akafanya mipango akahamishiwa kwingine, nikiwa na mimba changa nikamchukia sana mume wangu, sikuwa nataka hata tushirikishane habari za family na uchumi kama zamani, nilitamani hata kumtemea mate pindi nimuonapo. Kumbe alikuwa na tatizo la kiafya hakuniweka wazi.
Baada ya kujua nina mimba alianza kuniambia “mke wangu chunga sana” nikimuuliza kwa nini hajibu. Likawa neno la kujirudia. Kuna rafiki yake wanapatana sana, siku hiyo akanisimamisha njiani, akaniambia hongera shemeji naona umeokota waridi kwenye mchongoma, nikashangaa nikamuuliza maana yake nini? Akasema amefurahi kunitania hivyo.
Mimba ikaendelea kukua, mme wangu wala hana bashasha na mimi, rohoni namwambia unune ucheke itanyesha tu. Ndugu zake hakuna anayejishughulisha hata kunipa hongera, nikajua kuwa wote wanajua ndugu yao ana shida ya uzazi. Mume wangu akaanza kunipa maneno ya kashfa, kunisemesha maneno ya shombo hata tukiwa na watu, sikujali, nikajifungua mtoto wangu wa kiume, hapo ndipo vurumai lilianza.
Kipindi cha mwisho cha ujauzito alikuja dada yangu kunisikilizia, but toka amefika zaidi ya salamu mme wangu hakuongea naye chochote. Nilikwenda kujifungua hakufika Hospitali, nimetoka Hospitali hakutaka hata kumuona mtoto kwa sura, bahati njema alifanana na mimi.
Toka kipindi hicho mpaka sasa ni miaka miwili na miezi kadhaa, hatuna maelewano, hamtaki mtoto na haweki wazi sababu za kumkataa. Kuna baadhi ya rafiki zake naelewana nao sana, mmoja aliwahi kuniambia kuwa wakati mume wangu anasimamia biashara za baba yake alikuwa na jeuri ya pesa, mke wa mtu akajigonga kwake akamtafuna, jamaa akamfanya kitu kibaya akaugua ugonjwa wa ajabu ambao mwanzo hata ku erect ilikuwa vigumu.
Alifanyiwa dawa kwa waganga akapona ila vipimo vya hospitali vinaonesha kuwa hawezi kumpa mwanamke mimba sababu aliathirika sana viungo vya uzazi.Yeye mwenyewe na ndugu zake wanasemaga kuwa aliugua sana ila hiyo sababu ya kutafuna mke wa mtu hawasemi, wanadai baba yake alikuwa na ugomvi wa kudhulumiana mali na ndugu zake so wakamlogea mwanaye.
Nimewachosha sana Lakini hapa ninaomba ushauri. Je inafaa niendelee kuishi na huyu mwanaume kwa usalama wa mwanangu? Hajawahi kunitamkia moja kwa moja kwa moja kuwa mtoto sio wake, ila pia anasema nisimuite huyo mtoto kwa ubini wake.
Hajawahi hata kupakata, mtoto anajitahidi kumzoea lakini anamuwia kauzu mpaka mtoto keshajua, mtoto anaweza kushinda kwa furaha lakini akisikia honi ya gari la dady anakuwa mpole mpaka namhurumia. Some time najilaumu kwa maamuzi ya kumtafuta huyo mtoto kwenye haramu, sometime namlaumu mama yangu na wote walionishauri, sometime.. Sometime.. Sometimes zinakuwa nyingi kichwani kwangu, then najiambia ningeishi hivyo mpaka lini? Sometime naingiwa na ubinadamu namhurumia huyu mume, lakini najiambia ni kwa nini hakuniweka wazi tukatafuta alternative pamoja? kuna kipindi alianza angalau kumuonesha sura ya tabasamu, lakini saa nyingine mtoto akiharibu kitu anamkaripia mpaka najiskia vibaya.
Alifuta majina yake kwenye kadi ya mtoto ya clinic, nikamwambia kama hataki mtoto aitwe kwa jina Lake basi naondoka, akaniambia nisiondoke, zilikuwa ni hasira, nikamuuliza hasira na kadi au hasira na nani, akasema yameisha.
Nawaza sana wadau hasa kwa mustakabali wa mtoto, nifanyeje? Nimewaza kumweleza ukweli lakini nahisi nitakuwa nimempa majibu ya lile analo doubt. Na huenda nikampa kibali cha kumdhuru.
Ukijisikia kutukana shusha hata Tani 10, hapa ninawaza mpaka moyo umekuwa butu.
Wasalaam.