KUNA BINADAMU NA BINADAMU WANYAMA KWENYE MAHUSIANO, JIFUNZE
July 15, 2019
Edit
Kila mwanadamu aliyepitisha miaka 18, pamoja na mambo mengine anayoyatamani kwenye maisha yake, matamanio makubwa zaidi huwa ni kumpata mwenza sahihi wa maisha. Suala la kumpata mchumba ambaye mtaingia naye kwenye ndoa kwa kizazi cha sasa ni mtihani kidogo.
Wapo ambao wameufaulu, wanamshukuru Mungu lakini wapo ambao bado wanapambana ili siku moja na wao waingie kwenye maisha hayo ya ndoa. Unapotaka kuianza safari ya ndoa, kila mtu anaweza kukuambia lake kutokana na historia yake.
Kuna ambao watakuambia fanya haraka uoe maana umri unakwenda, kuna ambao watakukatisha tamaa kwamba wanawake au wanaume wa siku hizi hawana maana, bora kukaa peke yako nakadharika. Wapo pia watakaokwambia bora uzae tu uwe na mtoto hayo mengine ni majaaliwa.
Kwamba uhakikishe tu una mtoto au watoto wako wawili watatu basi. Haijalishi huyo uliyezaa naye atakuwa na msaada wowote au la. Ili mradi tu mtu uitwe baba au uitwe mama. Kuna ambao watakupigia mahesabu ya jinsi unavyotakiwa kuzaa vizuri na kuwalea watoto. Utasikia; “Zaa haraka bwana ili uweze kuwahudumia wanao ukiwa na nguvu sio unazaa umri ukiwa umeshaenda halafu unajikuta unashindwa kuwahudumia.”
Siwapingi wenye mtazamo huo lakini hapa nataka kukueleza kuwa, suala la kumpata mwenza wa maisha linahitaji busara, hekima ya hali ya juu katika kufanya maamuzi. Linahitaji umakini sana ili kuweza kufanya maamuzi ya kuingia kwenye ndoa na mtu sahihi.
Wengi sana wamekosea, wamejikuta kwenye matatizo makubwa sana kwa kuingia na watu ambao si sahihi. Unaingia kwenye ndoa na mtu ambaye ana roho ya kinyama. Hana ubinadamu, muda wowote anaweza kukudhuru, hili ni tatizo kubwa.
Bila shaka mimi na wewe ni mashahidi katika hili. Kwenye jamii zetu tunayaona haya. Siku hizi kusikia mke amemuua mumewe au mume kumuua mke imekuwa kama ni jambo kawaida. Watu wamepoteza utu, mioyo yao imekuwa kama ya wanyama.
Binadamu hawana hofu ya Mungu, bahati mbaya sana kwa macho yetu hatuwezi kujua mtu mwenye roho ya aina hii. Laiti kama mtu ungekuwa na upeo wa kujua moyo wa mtu ulivyo mapema, sidhani kama ungethubutu kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye
unajua huko mbeleni anaweza kukutenda jambo baya la kukudhuru. Hiyo ni siri kubwa, binadamu hatujui wenza wana mioyo ya aina gani. Hatujui mtu ana unyama wa kiasi gani. Ukimtazama kwa muonekano wa nje, unaweza kumuona ni kijana handsome sana, kumbe wapi ni hatari kama nyoka. Vivyo hivyo unaweza kumuona msichana mrembo, mzuri kumbe ni hatari kupita maelezo. Muda wowote anaweza kufanya lolote na kukatisha hata uhai wao.
Kikubwa ninachotaka kuzungumza na wewe leo ni kwamba, suala la mwenza wa maisha linahitaji neema kutoka kwa Mungu. Asikuyumbishe mtu kwa kukupa mifano ya njia zake, pita njia zako. Muombe Mungu akuo-neshe mtu sahihi katika maisha yako.
Kaa kwenye mazingira ya kumpata mtu sahihi, mchunguze tabia mtu unayetaka awe mwenzi wako wa maisha. Historia yake ikoje? Ana hofu ya Mungu? Hana historia ya unyama au kuwa na hasira za haraka ambazo zinaweza kufanya lolote muda wowote?
Kwa macho yetu hatuwezi, muombe Mungu akuoneshe mtu sahihi wa maisha yako. Akuna aliyemuomba Mungu mkate akampa jiwe, Mungu wetu ni mwenye huruma na anajibu kwa wakati, hawai wala hachelewi