KAMA HUNA BAHATI YA KUPENDWA , KWANINI UCHANGANYIKIWE?
June 12, 2019
Edit
MPENZI msomaji wangu, wiki iliyopita nilipata barua pepe kutoka kwa mmoja wa wasomaji wangu aliyejitambulisha kwa jina moja la Joanitha. Aliniandikia ujumbe mrefu sana juu ya kile kinachomsumbua kwenye maisha yake ya kimapenzi na akaniomba nimsaidie ili aweze kuwa na amani. Ujumbe wake huo ndiyo ulionisukuma kuandika makala haya.
Aliandika hivi: “Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 26. Nimekaa kwa muda mrefu sana bila kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume yoyote. Si kwamba napenda lakini nina kila sababu ya kusema, sina bahati ya kupendwa. “Niliwahi kumpenda kaka mmoja ambaye alikuwa akiutesa moyo wangu kwa muda mrefu. Nilishindwa kujizuia na siku moja nilipokutana naye nilimueleza bayana kilichokuwa kikiusumbua moyo wangu.
“Sikuwa tayari kumueleza moja kwa moja hivyo nilichokifanya ni kwamba, nilimnunulia kadi nzuri iliyokuwa na maneno makubwa yasemayo; ‘I LOVE YOU’ iliyokuwa na rangi ya kijani na nyekundu. (Kwa wasiojua, rangi hizo katika mapenzi zinamaanisha mapenzi ya kweli).
“Basi baada ya kumpatia kadi hiyo iliyokuwa imeambatana na maua, niliamini ujumbe wangu kwake wa kwamba nampenda umemfikia. Nilitulia kusubiri jibu. “Huwezi kuamini nilikaa takribani wiki mbili bila jibu lolote. Baada ya kukaa muda huo bila kupata jibu lolote nilibaini kuwa licha ya kwamba nilikuwa nampenda, yeye alikuwa hanipendi.
“Sikuishia hapo, nikatokea kumpenda kijana mwingine, naye ilikuwa hivyo hivyo. Sielewi nina kasoro gani. Mwenyewe nikijiangalia kwenye kioo najiona ni msichana ninayestahili kuwa na mpenzi lakini simpati wa kunipa faraja. Hivi jamani nina gundu gani? Naomba unisaidie anko.” Ujumbe huo uliniumiza sana. Nikajua wapo wasichana wengi sana huko mtaani ambao wanahitaji wapenzi lakini hawawapati.
Kuna wanaume ambao wanatokea kuwazimikia wasichana f’lani lakini kila wakijaribu kueleza hisia zao wanajikuta wanatolewa nje. Kimsingi hali hiyo imekuwa ikiwatesa wengi sana lakini sasa swali la kujiuliza; ni kwa nini inatokea hivi? Inakuwaje mimi natokea kumpenda msichana f’lani lakini yeye hana taimu na mimi?
Wanaojiuliza maswali hayo ni wengi na kupata majibu kwa haraka ni ngumu hasa kama huna elimu ya kutosha kuhusu mapenzi. Iko hivi, mapenzi yana kitu f’lani cha ajabu. Unaweza kushangaa anatokea mtu f’lani anakupenda sana lakini wewe huna taimu naye ila yupo ambaye na wewe unampenda sana lakini wala hakujali.
Lakini pia wataalam wa mapenzi wanaeleza kuwa, ni wachache sana waliopata bahati ya kuwapata watu wanaowapenda na ndiyo maana wengi wamebaki wakiumia kwa kutopendwa na watu waliotokea kuwapenda.
Watu kama hawa ndiyo wale ambao unawasikia wanaolewa na watu ambao hawawapendi, wanakubali tu kwa kuwa hawana jinsi. Matokeo yake sasa akiwa ndani ya ndoa kisha yule ambaye anampenda akajitokeza, ni rahisi sana kusaliti. Hata hivyo, wale wasio na bahati ya kupendwa kama ilivyo kwa Joanitha wanatakiwa kujua kwamba, mapenzi yanahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Unaweza kukaa muda mrefu bila kuwa na mpenzi lakini huwezi kujua Mungu ana sababu gani.
Huenda hao ambao wewe unawapenda lakini wao wanakupotezea, siyo wale waliopangiwa kuwa na wewe na endapo utalazimisha utakuja kujuta baadaye. Hatukatazwi kueleza hisia zetu kwa wale tuwapendao lakini tutarajie pia majibu hasi. Ujue kwamba huna haki ya kupendwa na kila utakayetokea kumpenda hivyo ikitokea umekosa uliyempenda, huna sababu ya kuumia.
Chukulia ni jambo la kawaida na huenda hiyo ndiyo safari ya kuelekea kumpata mtu atakayekupenda kwa dhati. Tuepuke kulazimisha kupendwa. Ukiona dalili kwamba unampenda lakini yeye hana chembe ya mapenzi kwako, kuwa mpole na muache. Nasema hivi kwa kuwa, wapo ambao wakitokea kupenda watafanya wawezavyo wafurahishe nafasi zao.
Hiyo ni hatari na nakuhakikishia kwamba, huwezi kupata penzi la kweli na badala yake utakuwa ni mtu wa kutendwa kila siku. Utasalitiwa, utaudhiwa na kamwe hutapata kile ulichokitarajia. Kwa nini? Kwa sababu uliyelazimisha awe na wewe, hakupendi kabisa.
Ukijaribu kufuatilia utagundua wengi wasioyafurahia maisha ya kimapenzi, wamepata bahati mbaya ya kuwapenda wasiowapenda lakini wakalazimisha kuwa nao. Ndiyo maana nikasema kwamba, ukiona huna bahati ya kupendwa, kubaliana na hiyo hali na wala usijione una kasoro au umelongwa. Fahamu muda wa kuwa na yule uliyepangiwa na Mungu haujafika na ukifika, utafurahi na roho yako.