HIRIZI YA MAPENZI SEHEMU YA 4 - Chumba Cha Mapenzi -->

HIRIZI YA MAPENZI SEHEMU YA 4

Mdharuba
*SEHEMU YA NNE*
“Kama utaamua kunipa hapahapa wewe nipe tu, lakini huko nyumbani mimi sirudi” Nilimjibu Rahel na kumwacha akishangaa.
“Ok, sawa, mimi narudi nyumbani, lakini leo umeniudhi sana..” Alilalama Rahel wakati anageuka kurudi alikotoka.
“Ukisema leo nimekuudhi unamaanisha siku zote nakufurahisha?” Nilimuuliza.
“Ndio, siku zote unanifurahisha, lakini leo sijui kwanini, lakini sawa, najua ni huu upendo wangu ndio unaokufanya uniringie”.
“Nyie wanawake ni wa ajabu sana, yaani siku zote nakufurahisha lakini hujaona hilo, umeona leo nilivyokukera, haya nenda salama”. 
“Samahani basi Jay, naomba nikuambie kitu” Rahel alisema haya huku akiniashiria niongee nae faragha kidogo, hakutaka Nira asikie alichotaka kuongea. Nilitii huku Nira akiwa amesimama pembeni akisubiri tumalize maongezi haraka ili tuwahi kutoroka tuepukane na janga liliokua mbele yangu.
“Hizi hapa pesa ulizohitaji, najua utakua na tatizo lakini hutaki kunieleza, ila nakupenda sana..” Aliniambia Rahel huku akifungua pochi yake na kunikabidhi noti za elfu kumi kumi nyingi. Wala sikuzihesabu, nilizichimbia moja kwa moja katika mfuko wa mbele wa Jeanz yangu na kuagana na Rahel kisha nikamgeukia Nira tukaondoka kwa mwendo wa haraka.
****************************************
“Umenibeba kama mwehu yani, hata sijui naelekea wapi” Nilimhoji Nira baada ya kuona tunaenda tu, sijui mwisho wa safari yangu.
“Twende kwa yule demu wako wa pale Makorora” aliniambia Nira.
“Wa Makorora yupi? Nasra, Regina au Rukia? Maana wako watatu pale Makorora” Nilimhoji Nira.
“Regina bana, ndo ambaye ana nafasi hiyo, Nasra si mke wa mtu yule, na yule Rukia muda huu yawezekana hata kurudi hajarudi”.
“Ok, hapo sawa, nimekupata”.
Tulifika hadi nyumba anayoishi Regina, hapakuonekana dalili kuwa kulikuwa na mtu mle ndani, milango yote ilifungwa kwa nje.
“Gonga basi bro” Nira aliniambia.
“Sasa nagongaje bro wakati milango imefungwa kwa nje hii, hapa hakuna mtu” Nilibisha kwa hoja. Kisha nikaongezea.
“Kwanini tusiende kwako tu? Tatizo nini kwani?” .
“Kaka, kwanza nahofia wanaweza wakawa wanapajua na kwangu, wewe ni 'best' yangu, kwahiyo lazima watu watakuwa wanajua tu ninapoishi kwa sababu muda mwingi tuko pamoja” Alinipa maelezo ambayo sikuyaafiki moja kwa moja.
“Wewe twende tu, unafikiri tutafanyaje saa hizi, wakija kunikamata basi tu” Niliamua liwalo na liwe.
“Hapana bro, hata hivyo mi mwenyewe nina mgeni pale kwangu, sasa unafikri tutalalaje watu watatu chumba kimoja kile?” Hii hoja ndiyo iliyoninyong'onyeza zaidi, nikaona nisimbishie Nira.
“Nina pesa ya kutosha amenipa Rahel, wacha nikalale gesti, kesho tutajua cha kufanya.” Maelezo haya yalionekana kueleweka mbele ya Nira, pasi na kuongeza neno alinisindikiza hadi gesti ya karibu na kuniacha pale yeye akaondoka.
****************************************
Nikiwa pale gesti ndipo nilipopata wazo la kumpigia Jacq nimueleze hali halisi, halafu nione kama anaweza kuja kubadili makazi na kuja hapa gesti. Simu iliita bila kupokelewa, nilipojaribu mara ya pili, ilipokelewa na kusikia sauti ya upepo kama mtu aliye katika pikipiki inayoendeshwa kwa kasi sana.
“Haloo, nipo kwenye bodaboda, naelekea nyumbani” Alinambia kabla ya kumwambia chochote.
“No, kuna gesti ya karibu nipo hapa, njoo bana, usiende nyumbani..” Nilijaribu kumsihi.
“Hapana, wamekufuatilia na wameshafika hapo gesti, acha mimi niwahi nyumbani, wewe enjoy usaliti wako, yaani uliona unikimbie uniache pale, looh.. Mfyuuu”. Jacq alimaliza kwa msonyo.
Nilipigwa na taharuki, nikachomoka pale ndani na kufungua mlango, nikaangalia kulia na kushoto, nikaanza kutimua mbio kuelekea geti la ile gesti.
Kabla sijalifikia, geti lilifunguliwa na kuingia askari watatu pamoja na mamaake Jacq (huyu namfahamu vizuri ingawa yeye hanifahamu) na mtu mwingine wa makamo.
Nikanyong'onyea sana., nikainama na kushika magoti yangu huku nikihema kwa nguvu sana..
“Nimekwisha, Mungu niokoe...” Nilijisemea moyoni.
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Itaendelea...