Kisa Cha Kusisimua: Nani Kama Mama..? - Chumba Cha Mapenzi -->

Kisa Cha Kusisimua: Nani Kama Mama..?


Kuna kijana mmoja daktari alikwenda kuposa. Binti aliyemposa akamuwekea masharti mazito.
Akamwambia chagua mawili ama kunioa mimi au kukaa na mama yako, kwa sababu ukinioa mimi sitokubali mama yako aje hata harusini kwangu! Yule kijana alielemewa. Hakujua la kufanya. Mke anamtaka, lakini mama yake pia anampenda. Hivyo aliamua kuomba ushauri kwa mwalimu wake wa chuo kikuu.
Alimwambia: moyo wangu unampenda mno binti niliyekwenda kumposa, lakini pia siwezi kuishi mbali na mama yangu. Nifanye nini?
Yule mwalimu mwenye hekima ambaye alikuwa anajua tabu alizopitia mama wa kijana yule, alimjibu kwa kumwambia: Kabla ya kukueleza uchague yupi kati ya wawili hao, rudi nyumbani, na leo usifanye chochote, ila kuiosha mikono ya mama yako. Yule kijana alifanya kama alivyotakiwa na mwalimu wake.
Alipofika nyumbani aliomba idhini kwa mama yake amruhusu kuiosha mikono yake, na yule mama alimkubalia bila ya hofu yoyote.
Yule kijana alipoanza kuiosha mikono ya mama yake na kuona jinsi ilivyogugutaa kwa kazi za sulubu, alilia sana. Muda wote huu alikuwa hajawahi kuangalia viganja vya mama yake.
Je, na wewe umewahi kukaa na kuangalia viganja vya mama au baba yako kuona tabu walizopitia kukulea?
Kumbe baba wa yule kijana alifariki dunia yeye akiwa bado mdogo, yule mama aliamua kusamehe kila kitu kwa ajili ya mustakbali wa mwanawe. Alijitolea kufanya kazi za sulubu. Alikubali kuwa mtumishi wa ndani, kukosha nguo, kupiga deki na kila kazi ambayo alihisi ingelimletea chumo la halali bila ya kujali ugumu wa kazi hiyo.
Juhudi zake zilizaa matunda na kufanikiwa kumlea na kumsomesha mwanawe hadi chuo kikuu na sasa ni daktari ambaye ana mustakbali mzuri.
Baada ya yule kijana kukumbuka yote hayo, alifanya haraka kumpigia simu mwalimu wake huku macho yakiendelea kububujikwa na machozi akimwambia, siwezi kusubiri hadi kesho. Jibu nimeshalipata.
Siwezi kumtupa mama yangu kwa ajili ya mtu asiyejua thamani ya mama. Ahsante sana kwa kunionesha njia sahihi! Kamwe siwezi kumuuza mama yangu kwa ajili ya leo yangu wakati yeye ameuza maisha yake yote kwa ajili ya mustakbali wangu.
NANI KAMA MAMA?!?
Tabasamu lako ni ufunguo wangu wa ufanisi.
Funzo: Kamwe usije mradhau mama yako na kutoona uthamani wake kwako eti kwasababu ya mtu baki..vitu ama mazingira Fulani..na kumsaliti..MPENDE SANA MAMA YAKO…MPENDE SANA BABA YAKO..NAWE UPATE KULA MEMA YA NCHI.