KILA SIKU UNAKIMBIWA NA WANAWAKE??....fungua usome hapa - Chumba Cha Mapenzi -->

KILA SIKU UNAKIMBIWA NA WANAWAKE??....fungua usome hapa


TUNAZU-NGUMZA kuhusu mapenzi, kama ilivyo kawaida ya ukurasa huu. Leo namalizia mada yangu niliyoanza wiki iliyopita. Ni kuhusu mambo ambayo wanawake wengi hawayapendi kwa wanaume zao. Inawezekana unashangaa kwa nini wanawake wanakukimbia kila siku, kumbe kuna sehemu fulani huwa unakosea bila kujua. Hapa ndipo kwenye dawa. Ndiyo sehemu pekee utakayoujua ukweli na kuchukua hatua.
Katika sehemu ya kwanza wiki iliyopita nilianza kwa kuelezea tabia mbili; moja ikiwa kujiangalia upya tabia zako na pili ni kumpa matunzo mwenzi wako. Nilifafanua kwa marefu na mapana kuhusu mambo haya lakini kwa faida ya wale ambao hawakubahatika kupata gazeti hilo, nitaelezea kidogo kuhusu kutoa matunzo.
Lazima wanaume mfahamu kwamba hata gari linapoharibika huhitajika kupelekwa gereji kwa kufanyiwa ukarabati. Vivyo hivyo hata mwanamke anahitajika kupewa matunzo ili aendelee kuwa bora na anayekuvutia. Ukweli ni kwamba, wanaume wengi hukwepa kutoa matunzo ya karibu kwa wapenzi wao wakidai wanachunwa! Nani amekudanganya ndugu yangu? Kumtunza mpenzi wako siyo kuchunwa!
Mpendezeshe apendeze, usipofanya hivyo wewe unataka nani akutunzie? Kama una tabia hii badilika haraka, maana wanawake wa sasa wapo makini kuangalia wanaume ambao wanatambua wajibu wao. Kuna mwingine huwa hatoi fedha mpaka siku atakayolala na mpenzi wake, hiyo ni mbaya zaidi maana hisia za kwamba umemnunua huanzia hapo.
Najaribu kuwaweka sawa na kuwakumbusha kwamba mwanamke anahitaji matunzo na kama ukishindwa kumtunza utakuwa unampa mwanya wa kutafuta mwanaume mwingine. Hapo ndiyo mwanzo wa usaliti.
UKOROFI, UKALI SI DAWA!
Watu wanatambua kwamba mwanaume ndiye kichwa cha nyumba, lakini hilo lisiwe kigezo cha wewe kuwa mkorofi na mjeuri hata kwa mambo mengine yasiyo ya msingi. Mwanamke anahitaji mwanaume mwenye msimamo, asiyeyumbishwa, lakini pia anatamani sana kusikilizwa mawazo yake. Mwanamke anahitaji kuliwazwa na mpenzi wake. Ukali kupindukia hupunguza mapenzi na hujenga woga na hofu. Wakati mwingine hushindwa kukushirikisha katika mawazo yake mazuri ambayo yangeweza kujenga kwa kuhofia ukali wako.
Ni vizuri kuwa makini katika hili, huna sababu ya kuwa mkali kwa mpenzi wako. Mwanamke ni mtu wa kuelewa, kama kuna mahali amekosea, zungumza naye taratibu huku upendo wa kweli, utii na utu ukionekana usoni mwako na hata kinywani mwako.
UAMINIFU
Kuna baadhi ya wanaume wana tabia ya umapepe, nikisema hivyo naamini naeleweka. Hili ni tatizo lingine wasilopenda wanawake. Siyo wanawake pekee bali hakuna mtu atakayejisikia vizuri mpenzi wake kuwa na tabia ya umalaya. Kila mmoja anapenda kuwa na penzi la peke yake na siyo la kuchangia! Ikiwa una tabia za kupenda kubadilisha wanawake kila wakati, tarajia kuachana nao kila siku.
Lazima mwanaume uwe na staha, mapenzi ya kweli na mtulivu kwa mwenzio. Naomba nieleweke kitu kimoja hapa, wakati mwingine hata tabia zako za ajabu ajabu, zinamkosesha raha mpenzi wako na fikra za kuachana na wewe zikizidi kuusumbua ubongo wake. Epuka tabia ya kusifia wanawake wengine vijiweni au ukiwa na mpenzi wako katika matembezi. Unapaswa kujiheshimu. Heshima unayoionesha kwa mpenzi wako ni kithibitisho tosha kwamba unampenda na kuheshimu uwepo wake.
MPE KIPAUMBELE
Mwanamke mwenye mapenzi ya kweli kwako, lazima atatamani kujua mambo mengi kuhusu wewe, lakini kubwa zaidi ni uwazi kuhusu maisha yake pamoja na kutoa ushauri kwako pale utakapohitajika.
Anapenda kuona ukimpa nafasi ya kwanza katika maisha yako, uwe wazi kwa kila kitu kinachoendelea katika maisha yako. Nafasi ya kwanza ninayoizungumzia hapa ni pamoja na kuwa naye karibu na kumpa taarifa za mipango yako ijayo, lakini katika hilo, pia, mwanamke anapenda kuona unaitambua thamani yake na kuyashika maisha yake ipasavyo.
Mwanamke akiona hapewi kipaumbele na mpenzi wake, hupoteza imani ya kuwa na mwanaume huyo. Kama una tabia hizi, ndugu yangu achana nazo, vinginevyo kila siku utaishia kubadilisha wanawake kama nguo. Mada yangu imeishia hapa kwa leo, tukutane wiki ijayo katika mada nyingine, USIKOSE!