Kwa Taarifa Yako Tu..Hiki Ndicho Ambacho Wanawake Huvutiwa na Kukipenda Kutoka kwa Wanaume ,Kama Huna Jitahidi Kuwa Nacho…!!! - Chumba Cha Mapenzi -->

Kwa Taarifa Yako Tu..Hiki Ndicho Ambacho Wanawake Huvutiwa na Kukipenda Kutoka kwa Wanaume ,Kama Huna Jitahidi Kuwa Nacho…!!!

Related image

Kama mwanaume lazima upate wakati wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya kulifanya penzi lako lizidi kuchanua.
USAFI BINAFSI
Asilimia kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana kukutana na mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya nyumba au la nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana usafi.
Mwanamke anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya ajiamini kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba safi. Hata anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia sebuleni hadi chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele.
KUJIAMINI
Mwanamke anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini – mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika. Suala la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia manukato mapya!
Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa kukuona ukiwa katika hali halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na mwenye kutoa maamuzi yasiyoyumba.
Wakati mwingine, mwanamke anaweza kukupima hata katika jambo ambalo amekosea yeye, ataangalia unavyotoa maamuzi yako, lakini pia atafuatilia kuona kama utakuwa mwepesi wa kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!
KUJITETEA
Kipengele hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni kwenye upande wa kujitetea zaidi. Wakati unapodai haki yako mbele ya mwanamke wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka wenye uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.
Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali inapobidi kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika hili, lakini mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi na ambaye yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’ ikiwa mtakutana na vibaka au watu wabaya wenye lengo wa kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.
Mwanaume aliye ‘fiti’ ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.
KUJALI
Wanawake wanapenda sana wanaume wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu na wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa sana ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.
UKARIBU
Kati ya vitu vinavyowapa mshawasha mkubwa wanawake ni pamoja na kusogezwa karibu. Hapa ni kuwa naye katika mambo mengi unayoyafanya kila siku.
Ni vizuri kuwasiliana naye mchana, ukitaka kujua aina ya chakula alichokula siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni mambo madogo sana lakini yanayoongeza nakshi katika mapenzi.
Yapo mengi sana ambayo kwa kuyafanya utakuwa umemsogeza mpenzi wako karibu yako. Hebu tumia ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za mwenzi wako kisawasawa!
KUMSIFIA
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na maana sana kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda kuwasifia wanaume zao. Nitakupa mifano miwili ya namna wanandoa wa jinsia mbili tofauti wanavyotambulishana kwa jamaa zao.
MWANAUME: “Peter kutana na mke wangu, anaitwa mama Diana. Nipo naye mwaka wa tatu sasa, tuna watoto wawili, huyo Diana na mwingine anaitwa Cris. Mama Diana, huyu ni Peter nilisoma naye A – Level, Tosamaganga Sekondari.”
MWANAMKE: “Suzan, huyu ndiye mume wangu mpenzi…anaitwa Elifaraja lakini mimi napenda zaidi kumuita Elly. Kiukweli nampenda sana mume wangu jamani, tuna mtoto wetu mmoja, anaitwa Agness. (Akimgeukia mumewe) Baby, huyu hapa ni rafiki yangu Suzan. Yaani tumekua naye mtaa mmoja huko Arusha.”
ANGALIA TOFAUTI
Bila shaka kwa namna wawili hao walivyotambulishana unaweza kuona tofauti kubwa. Mwanaume amemtambulisha mkewe kawaida kabisa, hajaonesha manjonjo au namna anavyompenda na kumthamini mwenzake, lakini mwanamke amefanya hivyo.
Sikia nikuambie, KUMSIFIA mwanamke, kuna nafasi kubwa sana kwake. Chunguza kwa makini, hata kunapokuwa na mgongano katika familia, halafu wakatokea wageni, baada ya utambulisho na mazungumzo ya hapa na pale, wageni wakiondoka kunakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumaliza mpasuko katika familia.
Jenga utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, unamuweka katika kilele cha upendo. Anajiona kamili, peke yake na mwenye nguvu kwako. Anajiamini na unamfanya azidi kukupenda kwa kuwa anaamini yupo na mwanaume ambaye anajivunia kuwa naye.
MALENGO
Wanaume wengi wana ulemavu mmoja; hawapendi kuwashirikisha wanawake katika mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri na wakati mwingine ikilazimika kumwambia mkewe basi kwa mshtukizo baada ya kukamilisha jambo husika.
Hii si sahihi. Dunia ya leo imebadilika rafiki zangu. Inawezekana wazee wa zamani walikuwa sahihi, maana ilikuwa ni suala la kununua ng’ombe na kuwaweka katika zizi kwenye kijiji cha jirani, halafu wanapewa malisho mazuri, baada ya miaka miwili wanazaliana, hapo ndipo anamweleza mkewe.
Siku hizi dunia imebadilika, kuna mambo mengi. Kuna suala la hasara katika biashara, utapeli n.k. Mkeo ndiye rafiki yako mkubwa kuliko wote, ndiye ndugu yako wa karibu zaidi kuliko yeyote. Yes! Mkeo ndiye ndugu yako maana umetengeneza naye familia. Mmeshirikiana kuzaa watoto na kujenga maisha pamoja.
Yeye anapaswa kujua mambo yako, ndiye mtetezi wako nambari wani. Mweleze juu ya malengo yako, wakati mwingine anaweza kukusaidia sehemu ambayo hukutarajia.
Hata hivyo, kumshirikisha katika malengo yako, kunampa nguvu na nafasi ya kujiona mama katika familia yenu. Msaidizi kamili wa nyumba yenu.
KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia. Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mkeo akawa katika hali hiyo, msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa wazazi wake anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako tu, kutampa matumani kwamba anaishi na mtu sahihi. Acha kupuuza mambo yake; hata yale madogo, kama ya ‘mtoto wa dada amerudishwa ada shuleni’.
Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza msaidie hata kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una tatizo binafsi, kazini kwako au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako, kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema. Kipaumbele kwa namna yoyote ile, kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.
TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya kirafiki kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha ndoa. Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda kwa mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake. Ni muhimu likaheshimiwa na kutengewa muda maalum wa kufurahia. Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume huwa si wafuatiliaji sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao. Wenyewe wanajiwazia wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.
Si sahihi.
Tendo la ndoa halina maana ya kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako. Ukiweza kumjulia mke wako katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo wake kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini nje wakati wewe ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?

Kuna kitu nimesahau kweli? Kama kipo nitafute pembeni, kwa hapa haya yatoshe kukufanya uelewe nilichotaka kukuelekeza. Nikuache na neno moja; uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo mikononi mwako. Ukitaka iwe shaghalabaghala, pia ni wewe tu!